TAFITI mbalimbali zinaonesha kuwa makampuni na nchi zenye kujali kipato cha mwananchi wake ndizo zinazofanya uzuri kibiashara, katika huduma, uzalishaji mali na uchumi mzima kwa ujumla.
Mathalani nchi kama Singapore, Malaysia, Bahrain, UAE, China, Brazil na kadhalika zimefanya mabadiliko makubwa katika mifumo yao ya uchumi kwa kugeuza meza zao juu chini, kwa maana ya kuanza kuwajali wananchi wao wazawa kuliko mgeni katika masuala ya mishahara na mapato kwa ujumla.
Ilivyo hivi sasa ni kwamba nchi zetu nyingi za Kiafrika ikiwemo Tanzania zimeghilibiwa na kudhani eti utaalamu toka nje, mitaji toka nje, ardhi na mali asili yetu eti vina thamani kuliko Mtanzania mzawa. Hili ndio kosa ambalo linatugharimu na litaendelea kutugharimu kiuchumi na kimaisha kwa miaka mingi ijayo kama lisiporekebishwa.
Ukweli ni kuwa rasilimali yetu ambayo ndio watu wetu ndio kitu chenye thamani kuliko kitu kingine chochote katika dunia hiii.
Rasilimali hiyo ili iwe na umuhimu na thamani kubwa zaidi ni lazima kwanza ipatiwe mahitaji yake yote ya msingi. Mahitaji hayo ni pamoja na chakula, maji, nishati, vifaa vya nyumbani, zana za kazi, mavazi, nyumba/malazi/makazi, kipando cha uhakika, elimu, maarfia na habari au mawasiliano ya aina mbalimbali kwa gharama nafuu na katika mfumo endelevu unaoyaweka mahitaji hayo katika vitu vya lazima na sio vya anasa.
Hali ilivyo sasa ni kwamba siasa na sera zetu za kiuchumi hazina mtazamo wala mwelekeo wa kuvipa kipaumbele vitu hivi na badala yake tumekamia kwanza kuwashibisha waliokwishashiba na kuishi kwa kutegemea misaada na mikopo toka nje bila ya kujali gharama kubwa watakazobeba watoto, wajukuu na vitukuu vyetu.
Baada ya mahitaji ya msingi ni lazima pia mwananchi ahakikishiwe usalama na ulinzi wa maisha na mali yake wakati wote ili awe katika hali ya kuchangia maendeleo ya watu na nchi bila hofu ya kudhurika au kunyang'anywa mali zake na wakora.
Hili linahitaji nchi yenye polisi walioajiriwa mahsusi kwa kazi hiyo na siyo kutaka wananchi wasiohusika na usalama na ulinzi kuwa na wajibu katika majukumu yasiyowahusu kwa maana yale wasiyolipwa mshahara kuwa kazi kwao.
Hali kadhalika, madhali wananchi wanalipa kodi ni lazima kuwe na polisi au wanausalama wa kutosha katika kila sehemu nchini tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo kufuatia kuvunjika kwa daraja la Vigunguti wezi wanaweza kufunga mtaa mzima na kuwaibia wenye maduka na hata kuua baadhi yao. Wizi wa hapa na pale unaweza ukavumiliwa lakini kuua huku nako askari wakishukiwa kuhusika ni jambo lisilostahili kukubalika kabisa. Mauaji yanayohusishwa na polisi yakizidi ipo haja ya kutafiti na kuelewa ni aina gani ya askari tulionao. Maana ukiwa na askari wezi na wauaji basi huna jeshi la polisi nchini. Katika hali kama hii wengi wataogopa kuwekeza na kujiingiza katika shughuli za uchumi na maendeleo kwa sababu wanajua fika ni mtutu wa bunduki utakaoamua hatima yao na sio utawala wa haki na wa kisheria.
Wakati ambapo wafanyakazi wataishi na kufanya kazi kama wapo wapo tu maana wanajua kutajirika katika nchi hii hakutokani na kufanya kazi kwa bidii bali kwa kuwa mwizi usiyekamatwa.
Mshahara wa mfanyakazi ni malipo ambayo yanastahili kuwa yale yanaofidia gharama halisi katika maisha yake na hivyo kumfanya asilazimike kufanya shughuli nyingine yoyote ila ile tu aliyoaajiriwa kwayo. Kinachotokea hivi sasa ni kuwa mwananchi analipwa mshahara wa elfu tisini wakati mahitaji yake kwa mwezi ni laki mbili au tatu.Je, katika hali kama hii mfanyakazi huyu ataacha kukopa na hivyo kujiingiza katika madeni zaidi ? Je, mfanyakazi huyu akipata mwanya sehemu ya kazi ataacha kuiba ili kufidia kile anachoona anapunjwa au kuibiwa ? Je, hapa kwa kweli mfanyakazi na mwajiri wake hawatakuwa wanadanganyana kwa maana ya kuwa, mfanyakazi atadanganya anachapa kazi na mwajiri atajidai analipa mshahara ?
Ni dhahiri kuwa bila mshahara halali na mujarabu kwa kila mfanyakazi na hususan wazawa katika nchi hii mageuzi, mabadiliko na mapinduzi ya kweli na ya kina kiuchumi na kijamii katika nchi yetu hayatakuwepo.